|
Mazishi Zanzibar
Mstari ulianza kupangwa taratibu. Minongono ya chinichini, vichwa kutingishwa kuashiria kukubali; hizo ndizo zilizokuwa ishara zilizotumika. Mistari miwili ya wanaume waliosimama wakitazamana kwa huzuni katika umbali usiozidi futi tatu. Wanaume wengine walikuja tokea pande zote mbili wakijiunga katika mistari sambamba na kuifanya irefuke zaidi, wakisimama bega kwa bega kwa kadiri macho yalivyoweza kuona. Polisi walitokezea. Wakajikusanya katikati ya njia na kusimamisha misafara yote. Magari na mabasi yalipaki pembeni. Watu waliacha mitaa myeupe. Wapanda baiskeli walishuka na kusimama au kutembea taratibu pembeni ya baiskeli zao kandokando ya kundi la watu wanaoangalia. Fundi mmoja wa kimasai aliyekuja na mabakuli ya mfinyanzi na akiwa juu ya baiskeli yake, aliendesha kuelekea katika mtaa akitokea mtaa wa nyuma. Alionekana kuchanganywa na hali aliyoikuta. Polisi wawili walimzuia. Mmojawao alitoa onyo kali, mwingine aliinama chini kufungua valvu ya tairi. Mara tairi lilikuwa tupu bila upepo, Masai naye akajiunga na msururu wa wale watembeao pembeni ya baiskeli zao. Ghafla tokea mbali na mstari kitu cha rangi ya kijani kiliweza kuonekana. Kimya kikatanda katika ule mkusanyiko wa watu. Lilikuwa ni jeneza. Kubwa sana na lilifunikwa kitambaa kikubwa cha kijani chenye michirizi ya dhahabu, kitu hicho kilitembea juu ya kundi la watu kama vile kilikuwa kinaelea. Karibu kilikuja na kila mmoja sasa aliweza kuona kwamba kilikuwa kimebebwa na mikono ya wanaume katika mistari. Wao hawakusogea bali walikikabidhi kutoka katika mikono yao na kwenda kwenye mikono mingine katika mstari huo mrefu. Kilisafiri kwa kasi ya ajabu, kikipita katika kundi la watu kwa urahisi hakuna hatari yoyote ingetokea. Kile kitambaa cha rangi ya kijani na dhahabu ya kungaa kilionekana kufunika sio mbao tu bali kitu fulani chepesi ambacho kilienda taratibu juu ya kundi la watu.
Sasa kilikuwa kando yangu. Wanaume waliokuwa katika mistari walisogea karibu pamoja, kila mmoja alijitahidi kukibeba japo kwa muda tu kile kitu wakati kikipita karibu yake. Wengine ambao hawakuwa karibu sana kiasi cha kutosha kubeba tokea chini, walikuja kwa pembeni angalau kugusa. Mikono ile ilionekana kukiongoza wakati kilipoanza kukata kona kali kuelekea kushoto na kisha chini ya barabara ya pembeni kuelekea katikati ya Jiji. Wanawake tokea madirishani na viwambaza hapo juu waliweza kuona kwa mara ya mwisho tukio hilo wakati likipotelea katika kona za mitaa karibu na Msikiti, ambapo ndipo palikuwa sehemu ya kumalizia safari. Hivyo ndivyo ilivyomalizika safari ya mwisho ya binadamu, mtu mkubwa. Mtu mkubwa, mcha Mungu, mwalimu mwenye busara aliyekufa nchini India baada ya ugojnwa wa muda mrefu. Maombi yake ya kurudi mara moja katika nchi yake aipendayo Zanzibar ilitimizwa siku hiyo katika Mji wa Mawe. Na Barghash 2001 Barghash@msn.com Imetafsiriwa na Mwalimu George Mwidima gmwidima@yahoo.com |